Mussa Azzan Zungu amechaguliwa kuwa Spika mpya wa Bunge la 13 la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Zungu alipata kura 378 kati ya kura 383 zilizopigwa na wabunge katika mkutano wa kwanza na kikao cha kwanza cha bunge la 13 la Tanzania. Kwa ushindi huo, Mussa Azzan Zungu anakuwa Spika wa nane wa Bunge hilo tangu kuanzishwa kwake, baada ya kuwashinda wagombea wa vyama vingine waliopata jumla ya kura mbili pekee. Zungu aliteuliwa na chama chake, Chama Cha Mapinduzi (CCM), kuwania nafasi hiyo, huku Spika, Dk. Tulia Ackson akijitoa katika kinyang’anyiro hicho kwa sababu ambazo hazikuelezwa wazi. Zungu, atasaidiwa na Daniel Sillo ambaye ameteuliwa kuwa Naibu Spika. Miongoni mwa waliowahi kushika wadhifa huo wa Spika katika historia ya Tanzania ni Adam Sapi Mkwawa, Erasto Andrew Mbwana Mang’enya, Pius Msekwa, Samuel John Sitta, Anna Makinda, Job Ndugai, na Dk. Tulia Ackson.