Wagonjwa wa Uviko-19 Waongezeka
Wizara ya Afya imetoa taarifa yake ambapo imeonyesha ongezeko la watu wenye maambukizi ya ugonjwa wa Uviko-19 nchini katika kipindi cha mwezi Februari hadi Aprili mwaka huu.
Takwimu hizo zimetolewa leo Jumanne Mei 20, 2025, na Ofisi ya Mganga Mkuu wa Serikali, Dk. Grace Magembe kupitia taarifa yake kwa umma, ambapo amesema kumekuwepo ongezeko la tetesi zinazohusiana na magonjwa ya mfumo wa njia ya hewa katika jamii nchini.
“Hali ya kuongezeka na kupungua kwa ugonjwa huu imekuwepo kila mwaka tangu kutangazwa kwa ugonjwa huu mwaka 2020. Kwa kipindi hiki ongezeko hili linaonekana zaidi katika Mkoa wa Dar es Salaam,” amesema Dk. Magembe.
Dk. Magembe amesema kupitia mfumo wa ufuatiliaji wa magonjwa ya mfumo njia ya hewa, wizara imebaini kuna ongezeko la wagonjwa wenye Uviko-19 kutoka wawili kati ya watu 139 waliopimwa Februari sawa na asilimia 1.4 hadi wagonjwa 31 kati ya watu 185 waliopimwa Aprili mwaka huu, sawa na asilimia 16.8.
“Tangu Februari hadi Aprili 2025, ufuatiliaji wa virusi hivi umeonesha ongezeko la visa vya UVIKO-19 kutoka asilimia 1.4 (wagonjwa wawili kati ya watu 139 waliopimwa) Februari hadi asilimia 16.3 (wagonjwa 31 kati ya 190 waliopimwa) Machi,” amesema Dk. Magembe.