Tanzania yaanza safari kuitambulisha Singeli kimataifa
Katibu Mkuu wa Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo na Msemaji Mkuu wa Serikali Gerson Msigwa amesema Serikali imedhamiria na imeanza safari ya kuupeleka muziki wa Singeli kimataifa, ili uorodheshwe katika utamaduni usioshikika kwenye Shirika la Elimu, Sayansi na Utamaduni la Umoja wa Mataifa (UNESCO).
Msigwa amesema hayo mkoani Dar es Salaam, wakati akifungua rasmi warsha ya Uteuzi wa Urithi wa Utamaduni Usioshikika iliyoendeshwa na UNESCO na kushirikisha wadau mbalimbali wa muziki, viongozi wa Serikali na wataalamu wa utamaduni.
Msigwa amesema muziki wa Singeli una uwezo mkubwa wa kuchochea maendeleo na kuleta umoja katika jamii ikiwa utazingatia maadili na kuakisi utambulisho wa Taifa la Tanzania.
Aidha, amelitaka Baraza la Sanaa la Taifa (BASATA) chini ya Katibu Mtendaji wake Dkt. Kedmon Mapana kuhakikisha linasimamia kikamilifu maadili katika muziki wa Singeli ili kuufanya uwe na hadhi inayostahili duniani.