Kanali Mamadi Doumbouya atangaza kugombea urais Guinea licha ya ahadi ya kutowania
Kanali Mamadi Doumbouya aliyenyakua madaraka Guinea kupitia mapinduzi ya kijeshi miaka minne iliyopita,atashiriki katika uchaguzi wa rais licha ya kuahidi hapo awali kuwa hatawania urais na atarejesha utawala wa kiraia.
Kanali Doumbouya aliwasili katika mahakama ya juu hapo jana Jumatatu akiwa amendamana na wanajeshi kuwasilisha rasmi azma yake ya kugombea urais.
Vyama viwili vikuu vya upinzani vimepigwa marufuku kushiriki katika uchaguzi huo unaotarajiwa mwezi ujao Desemba.
Waguinea walishangazwa na tangazo kuwa wagombea urais watahitajika kulipa ada ya dola laki moja kushiriki katika uchaguzi huo.
Mnamo Septemba mwaka 2021,mapinduzi ya kushtukiza ya kijeshi yalifanyika nchini Guinea nakumaliza hatamu yenye utata ya Rais Alpha Conde, chini ya mwaka mmoja baada ya kushinda muhula wa tatu uliogubikwa na maandamano mabaya na ukandamizaji mkali dhidi ya upinzani katika taifa hilo la magharibi mwa Afrika.