Watu 25 wameuawa katika mashambulio ya kijihadi Adamawa, Nigeria
Watu 25 wameuawa katika mashambulio mawili ya kijihadi katika jimbo la Adamawa, Kaskazini Mashariki mwa Nigeria.
Ripoti zinasema, mashambulio hayo yalitokea katika miji miwili ya Madagali na Hong inayopakana na Cameroon. Wanajihadi wa Boko Haram wanadaiwa kuhusika na mashambulio hayo kwa sababu wamekuwa wakidhibiti eneo hilo tangu mwaka 2009. Watu wenye silaha waliokuwa kwenye pikipiki walivamia soko katika mji wa Madagali na kuwauwa watu 21 papo hapo, huku idadi hiyo ikitarajiwa kuongzeka kwa sababu wenyeji wanasema watu wengine hawajapatikana. Mbali na mauaji hayo, watu hao wenye silaha, wameiba vyakula na pikipiki zilizokuwa kwenye soko hilo, huku watu wengine wanne wakipoteza maisha kwenye mji jirani wa Hong. Katika hatua nyingine, wanajihadi kutoka kundi la Lakurawa, wamewauwa waumini watano na kuwajeruhi wengine watatu, baada ya kushambuliwa kwa msikiti, katika jimbo la Kebbi, Kaskazini Magharibi mwa Nigeria.